Bakola ya Mdee yamkumba Makufuli
MWENYEKITI wa Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA), Halima Mdee, amebomoa ngome ya mbunge wa Chato, Dk. John Magufuli kwa kuzoa wanachama zaidi ya 300 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwa katika ziara yake wilayani Chato, Mkoa wa Geita.
Dk. Magufuli ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi, amejizolea umaarufu mkubwa nchini kiasi cha kujijengea taswira kwamba anaungwa mkono jimboni kwake, ambapo sasa kwa pigo hilo la Mdee, atapaswa kujipanga upya.
Akiendelea na ziara yake ya Kanda ya Ziwa ya kuimarisha chama na kuhamasisha wananchi waikatae Katiba mpya inayopendekezwa, Mdee aliwapokea wanachama hao wa CCM na kuwakabidhi kadi za CHADEMA kwenye mkutano wa hadhara uliyofanyika juzi katika viwanja vya stendi ya zamani.
Wanachama hao walieleza kuwa sababu iliyowasukuma kukihama chama hicho ni kutokana na kuchoshwa na kauli za kejeli za mbunge wao, Dk. Magufuli kila wanapomhoji kuhusu utekelezaji wa ahadi zake.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Christopha Masanja alisema kuwa wanakabiliwa na kero nyingi ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama licha ya kuwa karibu na ziwa Victoria, lakini kila wanapojaribu kumweleza mbunge wao, huishia kuwapa kauli za kejeli.
Akihutubia umati mkubwa wa wananchi, Mdee alisema kuwa serikali ya CCM imekuwa haiwathamini wananchi wake ndio maana imeshindwa kutoa kipaumbele kinachostahili katika kutatua kero zao na badala yake kuelekaza fedha nyingi kwenye mambo yasiyo na msingi.
Alisema kuwa sekta ya kilimo inayotoa ajira kwa Watanzania zaidi ya aslimia 80 imetengewa kiasi kidogo cha fedha kwenye bajeti ya mwaka huu
ya sh. bilioni 42 huku safari za rais zikitengewa sh. bilioni 50.
Mdee ambaye pia ni mbunge wa Kawe, aliwataka wananchi wa Chato kufanya mabadiliko na kuondoa uteja kwa CCM akisema kuwa licha ya kuwapa kura tokea nchi ipate uhuru lakini wameshindwa kuwatatulia kero zao.
Aliwataka kutorudia makosa hayo kwenye chaguzi zijazo badala yake wahakikishe kwenye ngazi zote za uwakilishi wanachagua wagombea watakaosimamishwa na CHADEMA.
Kuhusu Katiba
Mdee aliwataka wakazi wa Chato kuikataa katiba iliyopitishwa na Bunge Maalumu lililoongozwa na Samuel Sitta kwa kuwa halikuzingatia maoni ya wananchi walio wengi ambayo yalipendekezwa kwenye Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Aliwataka wawe makini propanganda za viongozi wa CCM na wafuasi wao wanaoipigia chapuo na kuinadi katiba mpya wakidai ni nzuri yenye kukidhi matakwa ya makundi yote.
“Licha ya katiba hiyo iliyopendekezwa kutumia fedha nyingi za wapiga kura zaidi ya sh. bilioni 100, bado katiba hiyo haikuweza kuzingatia maoni ya wananchi walio wengi yaliyopendekezwa kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba,”alisema.
Mdee alitaja baadhi ya maoni mhimu yaliyopuuzwa na Bunge Maalum kuwa ni maadili ya viongozi, tunu za taifa, Rais kupunguziwa madaraka, kutofutwa kwa nafasi za wakuu wa wilaya na mikoa, wabunge kuwa na ukomo na wananchi kumwajibisha mbunge wao akishindwa kuwajibika.
Mapema, Katibu wa BAWACHA Taifa, Grace Tendega, alisema kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu, ni wa muhimu kwani utasaidia kuking’oa madarakani CCM 2015.
Aliwataka wakazi wa Chato kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi huo huku akiwakumbusha kuwa uamuzi wao wa kuwachagua wagombea kutoka vyama vya CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD ndio utakaowaondolea dhuruma, adha na usumbufu wa michango isiyokoma.
Naye mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo, alisema inasikitisha na kushangaza kuona wilaya yao haina huduma ya maji safi na salama licha ya kuwa karibu na ziwa, huku mbunge wao akiendelea kujigamba kwa maendeleo ya barabara ya lami.
Mwenezi wa Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA), Edward Simbeye aliwataka vijana kuacha kulalamika na kunung’unika badala yake wachukue hatua ya kupigania haki zao kwa madai kuwa haki haiombwi.
Alisema kuwa vijana maskini nchini wataendelea kudharauliwa, kuonewa na kukandamizwa na mfumo mbovu wa utawala mpaka pale watakaoamua kuunganisha nguvu kukabiliana na hila hizo
No comments
Post a Comment