HATIMAYE, KESI YA CHONJI YASOGEZWA MBELE
MTUHUMIWA maarufu wa biashara ya dawa za kulevya jijini Dar es Salaam, Muharami Abdallah ‘Chonji’ (44), na wenzake wanne wameendelea kusota rumande baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuahirisha kesi inayowakabili ya usafirishaji wa dawa hizo hadi Novemba 19 mwaka huu
.
Mbali na Chonji, washitakiwa wengine ni Abdul Chumbi (37), Rehamni Umande (45), Tanaka Mwakasagule (35), na Maliki Maunda (29).
Kesi hiyo ilikuwa ianze kusikilizwa jana, ambako Wakili wa Serikali, Janeth Kitali mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Kaluyenda, aliomba itajwe tarehe nyingine kwani upelelezi bado haujakalimika.
Chonji na wenzake walikamatwa mnamo Oktoba 21, mwaka huu maeneo ya Magomeni Makanya alipokuwa anaishi, kutokana na kudaiwa kujihusisha na biashara hiyo ya dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride na Cocaine zenye thamani ya zaidi ya sh milioni 200, ikiwa kinyume na kifungu cha sheria ya dawa za kulevya 16 (b) sura ya 95 iliyofanyiwa marekebisho 2002.
Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi inayomkabili Mfanyabiashara maarufu nchini, Marijan Abubakar ‘Papa Msofe’ (50), na mwenzake Makongoro Nyerere, baada ya mshitakiwa wa kwanza Papaa Msofe kuwa mgonjwa.
Kesi hiyo imeahirishwa mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi hadi Novemba 18 mwaka huu.
Msofe ambaye kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani hapo Agosti 10, mwaka 2012 anadaiwa kuwa yeye pamoja na mwenzake Makongoro, Novemba 6 mwaka 2011 huko Magomeni Mapipa kwa kukusudia walimuua Onesphory Kitoli.
No comments
Post a Comment