KAMA UNATABIA HIZI SAHAU MAFANIKIO KATIKA MAISHA YAKO
Mara nyingi kila mmoja wetu anapenda kufanikiwa katika maisha yake. Hakuna ambaye hayapendi mafanikio kwa vyovyote vile. Kila mtu anapenda kuona mambo yake yakiwa mazuri siku hadi siku. Kutokana na hali hii, ndiyo husababisha sisi binadamu kujishughulisha kila siku ili kuweza kutimiza malengo yetu.
Pamoja na kila mtu kuwa anapenda mafanikio, lakini umeshawahi kujiuliza nini kinachoongoza hayo mafanikio na kuona wengine wanafanikiwa na wengine hawafanikiwi? Kama hujawahi kujiuliza, sitaki upoteze muda hapa kufikiria sana nitakupa jibu ili ikusaidie kusonga mbele zaidi.
Kitu pekee ambacho kinafanya wegine wafanikiwe na wengine washindwe katika maisha yao ni tabia tulizo nazo. Zipo tabia ambazo ukiwa nazo zitakupeleka kwenye mafanikio moja kwa moja, lakini pia zipo tabia ukizikumbatia zitakupeleka kwenye kushindwa na mwisho utajikuta unalaumu kwa nini iko hivi.
Katika makala hii inakupa mwanga na kukuonyesha tabia ambazo zinakukwamisha mara kwa mara kufikia malengo na mafanikio yako. Ukiwa na tabia hizi, sahau kitu kinachoitwa mafanikio katika maisha yako. Tabia hizi ni muhimu kwako kuzijua na kuziepuka, la sivyo zitakurudisha nyuma sana kila siku.(Soma Hizi Ndizo Fikra Zinazokuzuia Kufikia Viwango Bora Vya Mafanikio)
Hizi ndizo tabia zinazokuzuia kufanikiwa, kama unazo sahau mafanikio katika maisha yako.
1. Kama una tabia ya kukata tamaa mapema.
Maisha kwa jinsi yalivyo, ili tuweze kufanikiwa yanahitaji uvumilivu hali ya juu kwa chochote kile unachokifanya. Uwe unafanya biashara au umeajiriwa unahitajika pia uvumilivu mkubwa katika kufanikisha mipango na malengo yako muhimu uliyojiwekea.
Kama wewe una tabia hii ya kukata tamaa mapema katika maisha yako itakuwa ni ngumu sana kwako kufanikiwa. Hakuna kitu kinachoanza leo na kuleta matunda leo leo, muda unahitajika katika kufanikisha malengo yako uliyojiwekea. Acha kukata tamaa mapema sana, jipe muda katika mafanikio yako.
2. Kama unafikiri unajua kila kitu.
Ili uweze kufanikiwa na kufika katika kilele cha mafanikio unatakiwa kujifunza kila siku bila kuacha. Unapojifunza unapata vitu vipya vitakavyoweza kubadilisha maisha yako kuliko ulivyokuwa ukifikiri hapo mwanzo. Unaweza kujifunza kwa kujenga utaratibu wa kujisomea kila siku katika maisha yako bila kuacha.
Wapo watu ambao katika maisha yao si watu wa kujifunza. Ni watu wanaoishi maisha kwa kujifanya wanajua kila kitu. Kama unaishi maisha haya ya kutotaka kujifunza vitu vipya, hata kwa rafiki zako ujue kabisa kwako wewe itakuwa ni ngumu sana kuyafikia unayotaka. Tambua kitu kimoja muhimu watu wote wenye mafanikio duniani ni watu wa kujifunza kila siku.
3. Kama una tabia ya kutojiwekea malengo katika maisha yako.
Hautaweza kufanikiwa sana kwa kile unacholenga katika maisha yako kama hujajiwekea utaratibu wa kuwa na malengo. Ni vizuri ukajua wapi unakotoka, wapi ulipo na watu unapokwenda. Unapokuwa na malengo yanakupa nguvu ya mwelekeo na kujua hasa kule unakokwendwa katika maisha yako.
Jifunze kuwa na malengo yako binafsi, tengeneza vipaumbele kwa kuangalia yale malengo yaliyo ya muhimu sana, kisha anza utekelezaji. Usifanye kitu chochote nje ya malengo uliyojiwekea. Watu wengi wanakuwa wanashindwa kufanikiwa kutokana na kushindwa kujenga nidhamu binafsi katika malengo yao.( Soma Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja )
4. Kama una tabia ya kulaumu sana.
Wapo watu ambao maisha yao siku zote ni kulaumu tu watu wengine. Hawa ni watu ambao huwa wanaamini sana, matatizo yao mengi yanasababishwa na watu wengine. Hali hii ndiyo huwa inawapelekea kulaumu kila mara. Watu hawa wapo tayari kuilaumu serikali au kampuni wanazofanyia kazi pengine kwa huduma mbaya.
Kama una tabia hii ya kulaumu katika maisha yako, elewa kabisa utakufa maskini. Hii ni kwa sababu hakuna kitu au mabadiliko ambayo utakuwa unafanya zaidi ya kulaumu tu. Nguvu nyingi badala ya kuelekeza kwenye kutatua tatizo, unakuwa unazipeleka kwenye lawama. Mwisho wa siku utajikuta umevuna lawama hizo ambazo unazitoa.
5. Kama una tabia ya kupoteza muda.
Mafanikio yoyote yale unayotaka katika maisha yako yapo kwenye muda. Muda ulionao ni kila kitu, unaweza ukawa maskini au tajiri kutokana na jinsi unavyotumia muda wako. Wapo watu ambao katika maisha yao si watunzaji wa muda hata kidogo.
Ni mara ngapi umewahi kusikia au kuambiwa na rafiki yako twende mjini tukapoteze muda. Muda ndiyo kitu pekee ambacho ukiipoteza hautaweza kukirudisha tena katika maisha yako. Unataka kujuta katika maisha yako na uje kujiona hufai pale utakapo zeeka, endelea kupoteza muda wako. Ukiweza kutunza muda wako vizuri elewa utajiri ni wako.
6. Kama una tabia ya kuongea sana.
Kuna wakati wengi wetu huwa ni waongeleaji wazuri sana wa ndoto zetu na kusahau vitendo. Kama unaendeleza tabia hii ya kuongelea sana ndoto zako na huchukui hatua yoyote muhimu ya utekelezaji kuelekea kwenye mipango na malengo yako, sahau kuhusu mafanikio katika maisha yako.
Maisha hayahitaji uwe mwongeaji sana ili ufanikiwe. Maisha yanataka watu makini ambao hatua zao za utendaji zipo kwenye vitendo na sio mdomoni. Fanya chochote kile unachoweza ili kutimiza hatua zitakazo kusaidia wewe kutimiza ndoto zako. Acha kukaa na kusubiri kesho, maisha hayakusubiri.
7. Kama una tabia ya kuogopa kufanya mabadiliko.
Ili ufanikiwe na kuvuka hapo ulipo, unalazimika kufanya mabadiliko katika maisha yako. Hautaweza kuendelea mbele au kufanikiwa kama utakuwa unaendelea kufanya mambo yale yale kila siku. Kumbuka upo hapo, kwa sababu ya vitu ambavyo umevifanya kwa muda mrefu katika maisha yako siku za nyuma. Unataka mabadiliko, fanya vitu vipya.
Unaweza kubadilisha maisha yako ukiamua leo na sio kesho, kama unatabia hizo na bado unataka kuziendeleza katika maisha yako, sahau kuhusu mafanikio.
No comments
Post a Comment