VILIO VYATAWALA BUNGENI KIFO CHA MWAIPOSA
Mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, Eugen Mwaiposa ukiwasili kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma kwa ajili ya kuagwa jana. (Picha na Mohamed Mambo)
WABUNGE jana walikuwa na wakati mgumu kuzuia machozi kutiririka katika nyuso zao wakati jeneza lililobeba mwili wa Mbunge wa Jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam, Eugen Mwaiposa lilipokuwa likiingia katika viwanja vya Bunge kwa ajili ya mazishi.
Wengi wao wakiwa wamevalia vazi jeusi ikiwa ni alama ya maombolezo na wengine, hasa wanawake kuvalia khanga, waliangua vilio wakati mwili huo ukiingia viwanjani ukiongozwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM) aliyekuwa amebeba msalaba.
Haukuwa uso tu wa Bulaya ulioonesha kutatizwa, bali na mwili wake wote haukuwa sawa sawa, ukionesha kubeba majonzi makubwa kwa msiba huo.
Mbunge ambaye hivi karibuni alifiwa na mume wake Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Zabein Mhita (CCM) alionekana hajiwezi tangu mwanzo wa mazishi hadi mwisho akisaidiwa, dalili wazi akikumbuka uchungu wa kuondokewa na mtu wa karibu.
Magari ya mawaziri yakiwa yametangulia yakiongozwa na pikipiki na baadae magari ya wagonjwa, ambapo moja lilikuwa ndilo limebeba jeneza lenye mwili wa Mwaiposa yaliingia viwanja vya Bunge kupitia mlango wa watu muhimu.
Mara baada ya kufika, askari wa Bunge waliubeba mwili huo wakiongozwa na mbeba msalaba, ishara ya Wakristo, Bulaya hadi mahali pa kumwagia.
Mbunge Mwaiposa, aliyekuwa anawakilisha wananchi wa Ukonga kupitia CCM alikufa juzi akiwa usingizi kutokana na shinikizo la damu, ugonjwa uliokuwa unamsumbua kwa muda mrefu.
Kama wabunge walivyohangaika kwa majonzi na kulia baada ya tangazo la kufa kwa mbunge huyo alilolitoa Naibu Spika, Job Ndugai kabla ya kuliahirisha Bunge, ndivyo ilivyokuwa katika viwanja vya Bunge.
Kukiwa na utulivu mkubwa na vilio vya kimya kimya na vingine vya kwikwi, wabunge walisikiliza salamu mbalimbali kwa namna itifaki ilivyoruhusu.
Katika salamu zao za rambirambi, wazungumzaji waligusa mema yote aliyofanya Mwaiposa huku wakimtaja kama mwanamke shujaa, mwenye ukarimu, moyo wa kujituma na mchapakazi hodari.
Walisema alikuwa mtu wa watu huku akiwa rafiki kwa kila mtu akimuita dear (mpendwa). Ndugai alimweleza Mwaiposa kama mwanamke mchapakazi na anayethubutu, ambaye aliwania jimbo la Ukonga na kushinda.
Aidha Ndugai alisema alikuwa mwanamke aliye tayari kutetea na kulinda haki za wengine huku akiwa mstari wa mbele kujadili mambo yanayoletwa bungeni.
Ndugai alisema Spika wa Bunge, Anne Makinda amekatisha ziara yake Uswisi kurejea nyumbani, kuungana na wabunge katika maombolezo hayo na kusema Bunge limetoa rambirambi ya Sh milioni 5.
Akizungumza, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), Samuel Mshana alisema alisikitishwa mno aliposikia taarifa ya kifo cha mbunge huyo.
Katika hotuba yake, aliwataka watu kuweka matumaini kwa Mungu na kuwa na subira katika kipindi hiki cha majonzi. Mchungaji Mshana akimkariri Mwalimu Julius Nyerere aliwaambia kwamba heshima ya wabunge inatokana na huduma yao kwa umma kwa namna wanavyowawakilishi katika Bunge.
Wakati mtumishi huyo wa Mungu akitoa salamu za matumaini, pia aliwataka wabunge kuelekea katika uchaguzi wasiambatane na nguvu za giza ili kuchaguliwa na badala yake wamtumaini Mungu.
Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama alisema katika salamu zake kwamba kifo cha Mwaiposa ni pigo kubwa kwa CCM na Umma kwa ujumla.
Mhagama alisema mbunge huyo alikuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za wapigakura wake wa Ukonga na kutekeleza ilani ya CCM. Alisema serikali itashiriki katika msiba huo na kutoa rambirambi ya Sh milioni 5.
Mnadhimu wa upinzani Tundu Lissu, akizungumza kwa niaba ya kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe, alisema Mwaiposa alikuwa miongoni mwa wanawake 21 walioingia bungeni kupitia majimbo waliyoyagombania.
Akizungumza kwa sauti ya upole, Lissu alisema Mwaiposa alikuwa mwanamke shujaa, aliyeweza kutwaa moja ya majimbo yenye watu wengi katika jiji la biashara la Dar es Salaam na kuongeza kwamba hali hiyo pekee inamfanya kuwa mwanamke shujaa.
Mwenyekiti wa wabunge wanawake (TWPG), Anna Abdallah alimwelezea Mwaiposa kama ni mpendwa wao, mwanamke mwenye uthubutu na mlinzi wa haki za wengine hasa wanawake.
Alisema kundi lao, limetoa rambirambi ya Sh milioni 2. Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya serikali za mitaa na tawala za mikoa, Dk Hamisi Kigwangalla alimpa wasifu mkubwa Mwaiposa kwa kusema kwamba alikuwa mchapakazi, aliyekuwa na uwezo wa kufanya kazi hadi usiku ili kuhakikisha kazi inakamilika.
Mmoja wa wanafamilia, akitoa shukurani, alisema kwamba hawana cha kuwalipa bali Mungu mwenyewe. Mwaiposa anatarajiwa kuzikwa Jumamosi jijini Dar es Salaam.CHANZO:HABARI LEO
No comments
Post a Comment