HALI ya mambo inaelekea sio shwari ndani ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku utendaji kazi wa Katibu Mkuu wa chama
hicho, Dk.Wilibrod Slaa ukielezwa umekuwa
wa kupenda kusikiliza na
kukumbatia sana majungu na hatimaye kutoa maamuzi yenye chuki na upendeleo
dhidi ya wanachama na viongozi wasio na hatia.
Sanjari na hilo, baadhi ya viongozi wanadaiwa wameamua
kutumia mapungufu hayo ya uongozi na utendaji
aliyonayo kuwachimba na kuwamaliza wenzao ili kujiandalia mazingira ya
kukubalika na kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.
Habari za ndani ya chama hicho zimebainisha kwamba, kwa muda
mrefu sasa, uongozi wa Dk.Slaa umekuwa wa mabavu na jazba na hilo ndilo ambalo
limefanya hata wasaidizi wake wa karibu
akiwemo Naibu Katibu Mkuu, Mheshimiwa Zitto Kabwe ajiweke kando katika maamuzi
mazito yanayotishia mustakabali wa chama hicho.
Inaelezwa kuwa, viongozi wenzake ndani ya chama hicho
akiwemo Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Freeman Mbowe, wamekuwa wakimvutia pumzi Dk.Slaa kutokana na kuvunja protokali nyingi
ndani ya chama hicho ikiwemo baadhi ya viongozi na watendaji wa ngazi mbalimbali kutishwa na
wakitaka kujitetea wanaambiwa kuwa ni mamluki wa CCM wanaotumiwa na mafisadi.
Mathalani katika Jimbo la Kawe Wilayani Kinondoni ambalo mbunge wake ni Mheshimiwa Halima Mdee,
mambo yanaonekana kuwa si shwari kwa mbunge huyo baada ya kuwepo taarifa za vikao vya kumchimba na kummaliza mbunge
huyo vinavyodaiwa kuwa nyuma ya mchumba wa Dk.Slaa, Bi.Josephine Mushumbusi ambaye tayari amezaa naye mtoto mmoja.
Habari za siri kabisa zinasema, “Mama Slaa”, amekuwa
akitumia makundi ya vijana na wanasiasa wasioelewana na Mheshimiwa Mdee kuandaa
mikakati ya kumdhoofisha kisiasa ili kujitengenezea mazingira ya kulinyakua
jimbo hilo katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka 2015.
Vyanzo vyetu vimewakariri baadhi ya viongozi wa CHADEMA
wakielezea kufedheheshwa na kusikitishwa na mwenendo wa “Mama Slaa”, ambaye
analazimisha kuja juu ndani ya siasa za chama hicho na kutamani kukamata
madaraka kwa njia yoyote kwa kutumia mgongo wa Mzee Slaa.
Kiongozi mmoja aliyeomba jina lake lisitajwe amesema,
viongozi wa chama hicho wameingiwa na hofu ya chama hicho kuingia katika
mipasuko na migogoro kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu ujao, kwani viongozi
wengi walio katika tishio la kutemwa, wameapa hawatakubali na huo ndio utakuwa mwisho wa CHADEMA.
“Hebu fikiria…Mdee (Halima) anajisikiaje anapobaini “mke” wa
Katibu Mkuu wa chama ndiye anayefadhili na kuendesha michakato ya kumdhoofisha
kisiasa ili yeye apate fursa ya kugombea ubunge katika jimbo hilo?Unadhani
atalikubali (Mdee) hili kirahisi?
“Hapa ni wazi kutakuwa na mapambano makali ya siri na hadharani
, mapambano ambayo hayatamwacha salama Dk.Slaa. Watu wamepinda, wanasubiri muda
muafaka waanze kunyukana kisawa sawa”, ameeleza kiongozi huyo.
Kiongozi huyo alishauri kwamba, Dk.Slaa anatakiwa ampumzishe
nyumbani mtarajiwa wake Josephine na sio kuranda nae kwenye majukwaa ya kisiasa
na kumtia hamasa na uchu wa madaraka hadi kufikia kutaka kunyakua nyadhifa za
watu kinyume na demokrasia na muda ukiwa bado haujawadia.
“Lakini kwanini hili litokee, ni kwa sababu Dk.Slaa mwenyewe
amekuwa bubu mbele ya mama huyu na ukitaka ugombane nae mguse huyo mama
utashukiwa kama mwewe anayetaka kubeba kifaranga cha kuku”,alieleza kiongozi
huyo.
Kiongozi mwingine ametaka
viongozi wakuu wa CHADEMA, wachukue
tahadhari mapema badala ya kumwacha
Dk.Slaa akipangua safu za viongozi katika ngazi mbalimbali na wengine
kupendekeza watimuliwe uanachama kwa kisingizio cha kuimarisha chama kumbe
anakarabati himaya yake na watu wake.
Katika fumua fumua ya uongozi ambayo Dk.Slaa amekuwa
akiifanya, anadai anaifanya kwa mujibu wa Katiba ya CHADEMA ibara ya 7.7 na
kuwa anachukua hatua hiyo baada ya kubaini baadhi ya viongozi ndani ya chama
hicho hawana uwezo na wengine ni makada wa Chama Cha Mapinduzi.
“Kuanzia sasa naagiza makatibu wa wilaya kuniletea taarifa
za utendaji wa viongozi wanaofanya mikutano na wananchi, nitakuwa nawapima
kupitia mikutano hiyo pamoja na taarifa nitakazokuwa naletewa kutoka kwa watu
wangu, hatuwezi kujiandaa kushika dola wakati hatuna watu walio na dhamira ya
kuongoza wizara, mkoa, idara na vitengo vingine”, alisema Dk.Slaa akiwa kwenye
ziara ya Jimbo la Kigamboni mkoani Dar es Salaam mapema wiki hii.
Dk.Slaa alidai, amebaini baadhi ya viongozi wa chama hicho
hawajui itikadi, dhamira na lengo la
chama badala yake wapo wakishabikia chama bila malengo ya kweli huku wengine
wakiwa makada wa CCM.
Dk.Slaa hakuweza kupatikana jana kuelezea kama anazo taarifa
za ‘mkewe’ kuanza maandalizi ya kutengeneza mtandao wa kumng’oa Mbunge wa Kawe, Mheshimiwa Halima Mdee katika uchaguzi mkuu ujao, kwani
simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa, hata ilipopokelewa baadaye jioni,
mpokeaji alijitambulisha kama msaidizi wake na kusema Dk.Slaa yuko kikaoni.
Mheshimiwa Mdee naye hakuweza kupatikana jana kutokana na
simu yake kutopatikana.Jitihada za kumtafuta zinaendelea akiwemo “mama Slaa” ili kuwapatia habari
zaidi katika toleo letu lijalo
No comments
Post a Comment