KUNA usemi
usemao kuwa utasoma sana, utasahau sana na utajua machache (the more you learn,
the more you forget and less yo know)
Katika
harakati za kulaza chama cha Demokrasia, CHADEMA kumejikita katika kusaka
wafuasi na viongozi kutoka katika vyuo vikuu. Wenyewe wakiwa na imani kubwa
kwamba wasomi wataweza kukivusha chama vizuri hatimaye kushika dola.
Kwa bahati mbaya CHADEMA wamekosa ufahamu kuwa
wasomi ni makarani kwa kiasi kikubwa. Wasomi sio wanasiasa bali ni watendaji
wazuri wa ofisini. Na kauli hii inathibitisha na mwenendo mzima wa kisiasa wa
CHADEMA.
Pamoja na
kuwa wamepata mafanikio makubwa kukonga nyoyo za vijana wa vyuo vikuu, lakini
mikiki mikiki ya kisiasa bado inawapa shida kubwa.
Siasa
inahitaji watu makini na wenye vichwa vilivyotulia sio watu wa kucharuka
haraka. Na kwa msingi huo basi uongozi mzima wa CHADEMA umeshindwa kuweka
hadharani sera yao hasa ni ipi na ilani yao inasimama kitu gani, badala yake
wanachukua muda mwingi kuzungumzia ufisadi. Na kuchukulia ufisadi kuwa sera
halisi ya chama.
Katika
kipindi hicho hicho cha matengenezo ya ufisadi, CHADEMA watakaouchukua katika
kudhibiti ufisadi. Kwa hiyo chama hiki walipaswa kumueleza umati wa Watanzania
mbinu zilizo wazi ambazo wao katika utekelezaji wao watafanikiwa kuzuia
ufisadi, vinginevyo watakuwa wababaishaji tu ambao siasa zao zimejaa ulaghai.
Nasema
ulaghai kwa sababu pamoja na kuwa chama kimesheheni watu wenye digrii moja hadi
wengine wamesahau idadi ya digrii walizosomea, wameshindwa kutofautisha kauli
mbiu na ilani ya chama ambayo hufafanuliwa katika sera.
Kauli mbinu
zimejaa mpaka hawajui ipi itumike kwa kipindi gani. Walikuwa na operesheni
sangara hatujakaa vizuri tukaambiwa maisha magumu mara ukaibuka ufisadi tena
maandamano mpaka kieleweke.
Hali
haijatulia M4C. mikakati yote hii haiendi mbali kwa sababu haina Baraka katika
sera na ilani ya chama.
Leo
ukiwauliza wabunge wao ni kwa kiasi gani wametafsiri sera rasmi ya chama chao
sina uhakika iwapo watatoa jawabu moja lenye kufanana kwa mujibu wa sera ya
CHADEMA.
Au katika
majimbo walikochaguliwa ni kwa kiasi gani wabunge wametekeleza sera za chama
chao kulingana na ilani ya chama chao.
Wabunge na
viongozi wa CHADEMA sio wa kweli na pia sio waaminifu hata kidogo kwa sababu
katika mahubiri yao mengi wakiwa peke yao na wafuasi wao, huwadanganya na
kuwapotosha wafuasi wao eti serikali haijafanya lolote la maana kwa miaka yote
hamsini tangu ilipoanza kutawala.
Lakini
viongozi hao hao wanapokutana na kiongozi mkuu wa serikali Mhe. Jakaya Mrisho
Kikwete hupiga makofi mpaka idadi yake huwapotea. Baada ya kushangilia kwa
makofi na vigelegele, hufuatia mapambio ya kumsifu Mhe. Rais wetu Kikwete kuwa
anastahili pongezi na kuungwa mkono katika juhudi zake za kujenga uchumi wan
chi kwa kuimarisha mawasiliano kila mahali.
Mambo
mengine ya mapambio nimeyafahamu. Mfano hai ni pale Mhe. Rais Jakaya Mrisho
Kikwete alipokuwa ziarani Rombo na kule Hai. Mbunge wa Rombo Mhe. Selasini
(CHADEMA) alimwaga pongezi lukuki kwa Rais.
Baadaye kule
Hai kwa Mhe. Mbowe Waziri Mkuu kivuli na Mwenyekiti wa CHADEMA yeye tena katika
mapambio yake hayasemeki na haikutarajiwa maneno yale yatoke kinywani mwa
Mbowe. Lakini ndio hivyo ameyasema na watu tumeyasikia.
Swali la
kujiuliza kumbe uongozi wa CHADEMA mnajua mazuri ya serikali ya Jakaya Mrisho
Kikwete kwanini hawawaelimishi wafuasi wao hali halisi ya kisiasa kwa upande wa
serikali na wao CHADEMA wanatofautiana nini au kwa upande upi na serikali?
Haya
hayasemeki kumbe siasa za CHADEMA ni za woga. Wakiwa peke yao wamesema mengine wakikutana
na hao wenye serikali yao wanasifu mengi.
Kimsingi
uongozi wa chama hiki wote wana ndimi mbili. Hazijulikana ni ulimi upi husema
lililo la kweli na ulimi upi na upande gani husema yaliyo na uongo.
Babu yangu
alinisimulia hadithi wakati huo wa kukaa na kucheka na babu kwamba nyani akiwa
porini na wanyama wenziwe basi nyani husimama kwa miguu miwili na kuwakoga
wanyama wenzake kwamba yeye ni binadamu.
Lakini,
atakapo tokea binadamu wa kweli nyani hurudia unyama wake na kutembea kwa miguu
na mikono. Kwa kufanya hivyo wanyama wenzake humdhihaki kuwa nyani sio lolote
wala chochote kumbe mwoga kuliko kunguru.
Hivyo,
uogozi wa CHADEMA mbele ya viongozi wa serikali na CCM huwa wadogo wakiamini na
kutii kama wafanyavyo raia wengine na kuthibitisha kuwa wao ni viongozi bandia.
Rais Kikwete
alisema kuwa yeye ndio Rais wa Tanzania na nao CHADEMA hawana Rais mwingeni na
hawana kwa kwenda isipokuwa kwake. Kweli leo CHADEMA wale wale waliosema mpaka
kieleweke na wataandamana bila ya kikomo, sasa wanamuimbia mapambio Rais
Kikwete.
Kwanini
CHADEMA wanashindwa kutunga na kujenga hoja kupitia sera za chama chao. Kwa
sababu wamejaza ‘madeski ofisa’ sio wanasiasa hivyo hoja za kisiasa CHADEMA
zinakosa majibu yaliyo sahihi.
Ukosefu wa
sera kwa chama kupelekea mapungufu yanayopatikana. Kwa kukosa sera CHADEMA
wanakosa majibu kwa serikali juu ya matatizo mbalimbali yanayojitokeza hapa
nchini.
Ukifuatilia
kwa karibu hoja za CHADEMA zote zimejaa lawama na malalamiko bila ya kutoa
jawabu mbadala la mtatuzi wa matatizo yanayojitokeza. Wamejikita kwenye itikadi
za uliberali lakini kilichowazi ni kwamba huko wamefuata masilahi tu.
Wao CHADEMA
walijua fika kwamba ukijichanganya katika makundi utafanikiwa kupata misaada
kutoka nje na kufanikisha mambo yako. Lakini, kinyume cha masilahi binafsi
kutoka katika jumuiya waliberali hatujawasikia CHADEMA wakiueleza umma wa
Watanzania uliberali unataka nini kijamii, kisiasa, kiuchumi na utamaduni.
Nina imani
kubwa kabisa hata Dk. Slaa, Marando, Tundu Lissu, Prof. Safari, Prof. Baregu
hawajaota iwapo wao wanawajibika kuwafundisha uliberali wana CHADEMA.
Hivi Erasto
Tumbo kule Meatu au Baradi wanajua madhara ya uliberali? Je Bw. Singo kule
Bomba mbili au Mfaranyeki wanajua sera ya uliberali au Bw. Mnyika Manzese Sinza
na Ubungo wanayo taarifa juu ya sera ya uliberali?
Rasilimali
maji ugawanyo wake ukoje kiliberali. Sasa utaona hakuna hata kiongozi mmoja
ndani ya CHADEMA hata Mwenyekiti wao mwenye dhamana ya kuisimamia sera ilani na
katiba anaeizungumzia sera ya uliberali.
Sina uhakika
iwapo itikadi ya uliberali imo au imeingizwa katika katiba ya CHADEMA na kama
imeingiziwa ni kiasi gani cha uelewa wa wana CHADEMA juu ya sera itikadi ya
chama chao.
Vinginevyo
ufisadi M4C kugeuzwa sera itikadi ilani itakuwa wamewatapeli wazungu wanaotoa
nguvu zoa kwa kuamini zinafanya kazi kumbe huku zinakwenda kushoto kulia.
CHADEMA
semeni sera yenu itambulike ili ikosolewe ikibidi. Kauli mbiu sio sera. Jibuni
hoja za kisiasa kwa sera za chama chenu ili mwelekeo na matarajio yenu yawe
wazi.
Kumbukeni
usemi njia ya mwongo ni fupi kwa kukosa sera hata mkibahatisha kuingia Ikulu
mtaingia mlango wa mbele mtatokea mlango wa nyuma papo hapo.
ends
No comments
Post a Comment