Header Ads

Breaking News

CHADEMA SASA KUMTIMUA SHIBUDA



BAADA ya kuwatimua  uanachama madiwani  watatu katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza hivi karibuni, Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),imepanga kupitisha azimio la kumtimua uanachama Mbunge wake wa Maswa Mashariki, Mheshimiwa John Magale Shibuda kwa kile wanachodai kuwa ni mtu hatari ndani ya chama hicho anayetumiwa na CCM.



Habari za uhakika kutoka ndani ya sekretarieti ya chama hicho ambayo ndiyo inayoandaa agenda za Kamati Kuu  zimesema,  agenda ya kumtimua Shibuda rasmi ndani ya chama hicho imekamilika kwani taarifa ya uchunguzi  wa tuhuma mbalimbali dhidi yake,  imekamilika na itawasilishwa pamoja na mapendekezo yake ndani ya kikao hicho.



Mpasha habari wetu amesema, kikao hicho muhimu  kitakachoamua pia mustakabali  wa baadhi ya viongozi wa kisiasa wakiwemo madiwani wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali ya kimaadili zimesema, uongozi wa juu wa chama hicho umechoshwa na mwenendo wa kisiasa wa Mheshimiwa Shibuda na wameona hawana njia nyingine zaidi ya kumfukuzia mbali.



Imeelezwa na viongozi hao kuwa, pamoja na Shibuda kujitoa CCM na kujiunga na CHADEMA mwaka 2010 baada ya kufanyiwa mizengwe, bado ameendelea kuienzi CCM na  kuwa na mahusiano na mashirikiano ya karibu na baadhi ya makada na viongozi muhimu wa CCM na serikali akiwemo Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Mrisho Kikwete.



Wamesema, kauli na matamshi mazito ya Shibuda kuhusu kambi ya upinzani na CHADEMA kwa ujumla, hayatoi taswira na mwelekeo sahihi wa chama hicho mbele ya wapigakura wao badala yake inakionyesha chama hicho kuwa ni chenye migawanyiko na viongozi wasio na msimamo.



“Ni wazi Shibuda bado yuko CCM, alipitia tu CHADEMA ili kupata ubunge wake baada ya kule kwao kuwekewa mizengwe. Huyu hatufai hata kidogo, lazima atoswe kwa gharama yoyote. Ni bora tukalipoteza jimbo hili badala ya kuendelea kuwa na aina hii ya mbunge anayetuchimba bila woga kwa kupewa Baraka na CCM”, Mpashahabari wetu amemkariri Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Mabere Marando ambaye ndiye aliyepewa jukumu la kuendesha tume ya uchunguzi dhidi ya Shibuda.



Mheshimiwa  Shibuda amekuwa ni mbunge pekee wa CHADEMA aliyejipambanua hadharani kukosoa msimamo wa wabunge wenzake wa chama hicho kugomea posho, akisema wanaogomea posho hizo ni kwa sababu wana ukwasi(utajiri)  mkubwa wa fedha kwa hiyo, kwao posho si lolote, lakini kwa mbunge maskini kama yeye na anayetegemea kwahudumia wapigakura wake, bado posho wanazolipwa wabunge ni ndogo na zinastahili ziongezwe.



Aidha,  Mheshimiwa Shibuda amekuwa akikemea ukabila ulioshika kasi ndani ya CHADEMA na kuhoji kama kuna uhalali wa hata nafasi ya Katibu wa Wilaya wa chama hicho katika mkoa ambao hauna asili ya uchaga, kulazimisha lazima ishikiliwe na Mzawa wa Mkoa wa Kilimanjaro.



Mheshimiwa Shibuda  alihoji mambo hayo kuwa, hayakijengi chama hicho zaidi ya kuzidi kutoa picha mbaya mbele ya umma na hivyo kuyapa turufu madai ya wapinzani wao ambao wamekuwa wakipiga kelele kila siku kuwa CHADEMA ni chama cha Wachaga.



Katika siku za karibuni, Mheshimiwa Shibuda alizidi kuwakoroga viongozi wa juu na wanachama wa chama hicho pale alipoibuka katika mikutano muhimu ya CCM na kupewa fursa ya kuhutubia na kisha kukumbatiana na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.



Mkutano wa kwanza ni ule uliofanyika Makao Makuu ya CCM Mjini Dodoma (White House), ambapo Mheshimiwa Shibuda aliibuka na kutangaza nia yake katika mkutano huo kuwa, atagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CHADEMA na Rais Jakaya Kikwete ndiye atakayekuwa mpigadebe wake.



Aidha katika Mkutano Mkuu wa CCM Taifa uliofanyika Kizota mjini Dodoma mwezi  Novemba mwaka huu, Mheshimiwa Shibuda alikuwa mmoja wa waalikwa na kwa nafasi ya pekee, aliwahutubia wajumbe wa mkutano huo wa CCM na kuwapa somo la kutaka waamke kutoka usingizini.



Alipoongea na gazeti hili hivi karibuni kuhusiana na msimamo wa yeye kwenda kuhudhuria mkutano huo wa CCM, Mheshimiwa Shibuda alisema, alikwenda kwenye mkutano huo sio kuiwakilisha CHADEMA bali alikwenda kuiwakilisha taasisi anayoiongoza ya African Peer Review Mechanism (APRM) huku agenda inayomsukuma ikiwa ni ya utaifa kuliko kitu chochote.



Shibuda alisema, utaifa wa Tanzania sio CHADEMA  bali kwake Utanzania ndio msingi muhimu na hasa anapoangalia taifa lilipotoka, lilipo na linapoelekea.



Alisema, mbali ya kuwa mwanasiasa mkongwe, ni mtaalam wa michakato ya uongozi na utawala bora inayoratibiwa na asasi yake ya APRM na kutokana na sifa hiyo, pamoja na kuwa mpinzani , ameamua kuwagutua CCM ili wajue wanakotaka kupelekwa .



“Nimeweka mgutuko kwa CCM ambao umewasaidia kuwapa fursa ya kujisahihisha na kuwajengea uwezo wa kujitathmini kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao”, alisema Shibuda na kuongeza kuwa alifanya hivyo kutokana na ukweli kwamba CCM ndicho Chama Tawala.



Kauli hiyo ya Shibuda na nyingine ambazo amewahi kuzitoa, zimekuwa zikiwachoma na kuwatia kiwewe viongozi wa chama hicho ambao wameahirisha mara kadhaa  mpango wa kumshughulikia, lakini hivi sasa wameapa ama zake ama zao.



Shibuda  hakupatikana jana kuelezea  taarifa hizi za kumtimua ndani ya chama hicho kama anazo kwani simu yake ilikuwa ikiita bila majibu, hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, hakuujibu ujumbe huo hadi tunakwenda mitamboni.  

No comments