Vigogo wa upinzani matatani Washinikizwa kurejesha kadi za CCM
Vigogo wa upinzani matatani
Washinikizwa kurejesha kadi za CCM
TAKRIBAN viongozi wote wa kitaifa kambi ya upinzani
wameanza kutafuta njia ya kujinusuru ili kuthibitisha ukweli wao baada ya
Katibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani kuthibitisha bado ni mwanachama hai wa
Chama Cha Mapinduzi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili tangu Katibu
Mwenezi wa CCM Bw. Nape Nnauye aeleze kwamba mwenzake wa CHADEMA Dk. Wilbrod
Peter Slaa ni mnafiki anabeba kadi ya vyama viwili vya siasa vigogo kadha
wameanza kukutana kupanga mikakati ya kujieleza wakiibuliwa.
Dk. Slaa hakupenda kupoteza muda wa jamii kukanusha
bali aliripotiwa kukiri uanachama wa CCM, lakini anasema kadi hiyo ameamua
kubaki nayo kama kumbukumbu yake.
Ameshindwa kusimamia ushahidi wake anaotoa kila mara
kutaka wanachama wa CCM wapeleke kadi zao CHADEMA wanapoamua kukimbilia
upinzani badala ya kudhihirisha walikozipata au kubaki nao kama alivyofanya.
Kiwewe hiki pia kimezingira majaliwa ya Mwenyekiti wa
TLP Bw. Agustine Lyatonga Mrema ambaye naye aliwahi kukiri miaka 12 iliyopita
kwenye kipindi cha Kitimoto kwamba anayo kadi ya CCM yaani hajakana ukereketwa
kwa vitendo.
Kwa mtiririko huo Bw. Mrema ni mwanachama wa vyama
vitatu vya siasa ambayo ni CCM, NCCR-Mageuzi na sasa TLP ambako huko ni Mwenyekiti.
Hakuna kumbukumbu rasmi za kuonyesha kwamba Profesa
Ibrahim Haruna Lipumba wa CUF aliwahi kurudisha kadi ya CCM alipoacha kazi
mwaka1994 kumshauri Rais na kukimbilia mrengo wa kushoto.
Ungamo la Dk. Slaa litamuweka pabaya Profesa Lipumba na
Maalim Seif Sharif amekuwa mstari wa mbele kuikaba serikali ya CCM wakati naye
ni mmoja wa wafuasi wa chama hicho.
Huko NCCR-Mageuzi, UPDP,SAU,TADEA, ADC naUDP vikao vya
siri vinaendelea kuzima azma ya Bw. Nape kuwafichua wanaojidai mitaani usiku
kwa kutumia kadi za CCM lakini mchana huibuka na kujifanya ni vinara wa kutetea
wanyonge kwa majoho ya upinzani.
Bwana James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, John Momose Cheyo (UDP),
Fahmi Dovutwa (UPDP) Paul Kyara (SAU) Saidi Miraji (ADC) na John Chipaka wa
TADEA wanajulikana kuwa hawajachoma mbeleko ya CCM bali wanajipa moyo kubaki
upande usiokuwa na tija.
Katika mahojiano na wanasiasa kadha idadi kubwa
wamemtaka msajili wa vyama vya siasa atoe ufafanuzi kuhusu watu wenye kadi za
vyama vya siasa zaidi ya kimoja hasa inapotokea mtu anagombea urais, ubunge na
udiwani.
Kundi jingine limesema huo ni unafiki mtu mzima kukosa
uamuzi wa kujua chama anachofuata hivyo wale vigogo wanaobainika wachague moja
kubaki upinzani au warudi walikotoka.
Jeuri ya viongozi wa CHADEMA kudandia hoja na
kupindisha ukweli imeota mbawa lilipojitokeza suala la Katibu Mkuu wao
kuthibitisha anatii kanuni za vyama viwili CCM na CHADEMA ambayo haviwezi kukaa
meza moja kwa hali yoyote.
No comments
Post a Comment