AUAWA KISHA KUNYOFOLEWA SEHEMU ZA SIRI
Watu wasiofahamika wamemuua kwa kumkata mapanga na kisha kumnyofoa sehemu zake za siri mkazi wa Kijiji cha Kanegele, wilayani hapa, Mkoa wa Geita, Hollo Machibula (54).
Akizungumza kijijini hapo juzi, Diwani wa Kata ya Bukandwe, Henry Alphonce alisema Hollo alivamiwa na watu hao nyumbani kwake juzi saa 5:00 usiku akiwa amelala na kuanza kumkatakata kwa mapanga.
Alphonce alisema mwanamke huyo alikuwa akiishi na binti yake, Tatu Juma (25) ambaye wauaji hao walimlazimisha kuingia chini ya uvungu wa kitanda kabla ya kuanza kumshambulia mama yake.
Alisema alipata taarifa za tukio hilo saa 6:00 usiku baada ya kupigiwa simu na viongozi wa kitongoji waliofika eneo la tukio na kushuhudia mauaji hayo.
Mtoto huyo alisema alishuhudia jinsi mama yake alivyokuwa akichinjwa na kunyofolewa sehemu zake za siri walizotoweka nazo wauaji hao.
“Waliniamrisha nilale chini nisiwaagalie usoni, walipomaliza kumchinja mama walikimbia na mimi nikapata mwanya wa kupiga kelele kuomba msaada nikiamini kuwa mama atakuwa kaumizwa tu hajafa,” alisema Tatu.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo walidai kuwa huenda chanzo cha mauaji hayo ni migogoro iliyokuwapo kwenye ndoa ya binti yake na mumewe.
Inadaiwa kuwa Tatu alikorofishana na mumewe ambaye hawakumtaja jina na mume huyo alipokuwa akienda nyumbani hapo kumtaka arudi nyumbani kwake, mama yake alikuwa akimkataza binti huyo asirejee kwa mumewe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema wanamshikilia mtu mmoja kwa mahojiano na wanaendelea kuwasaka wale wote waliohusika na mauaji hayo.
Alitoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuisaidia Polisi kuwasaka wauaji hao.
via>>Mwananchi
No comments
Post a Comment