Wenje: Waziri kutolewa kafara ufisadi escrow
Dodoma. Pamoja na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kueleza kuwa hajakabidhiwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuhusu uchotaji wa Dola 200 milioni katika akaunti ya escrow, Bunge limeelezwa kuwa kuna waziri mmoja ambaye anaandaliwa kisaikolojia kwa ajili ya kutolewa kafara.
Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje alisema hayo
jana wakati akichangia hoja ya mpango wa maendeleo ya Taifa mwaka
2015/16 akisema kuwa mipango mingi inashindikana kutokana na kukithiri
ufisadi.
Alitolea mfano wa ripoti ya escrow kwamba wabunge
waliomba iundwe tume, Serikali ikakataa ikidai haijapata ripoti bila
kueleza itapatikana lini.
“Ripoti ya Takukuru imeisha ili tujadili, lakini
taarifa tunazopata leo kwamba kuna naibu waziri mmoja mdogo huko Dar es
Salaam anaandaliwa kisaikolojia ili aje atolewe kafara hapa, haki ya
mama hii kitu mpaka ing’oe bati,” alisema Wenje.
Wenje pia alipinga kitendo cha Serikali kwenda
kuomba misaada nje huku ikiwa na mzigo wa mawaziri kiasi kwamba hadi
kuna mawaziri wasio na kazi maalumu akihoji ni jinsi gani Serikali
inaweza kupunguza gharama kwa kuwa na mtindo huo.
“Haiwezekani unakwenda kuomba msaada kwa wizara
23, halafu una mawaziri 50. How do we cut down cost (Tutapunguza vipi
gharama)? Alihoji Wenje huku akipinga mpango wa maendeleo uliowasilishwa
na Serikali kwamba hautekelezeki.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila akijadili
mpango huo, alisema haiwezekani ripoti ya escrow hadi sasa
haijawasilishwa ili ijadiliwe wakati kuna ufisadi mkubwa uliofanyika.
“Nimezungumza mwaka jana nimezungumza juzi na leo (jana) kwamba
haiwezekani watu wachache wazuie kupatikana fedha kutokana na ripoti
hiyo.
“Hatujui ripoti itatoka lini na suala liko vipi. Haiwezekani familia tano au 10 zizuie tusipate fedha,” alisema Kafulila.
Hoja za wabunge hao zilikuja baada ya Pinda
kulieleza Bunge katika kipindi cha Maswali ya Papo kwa Hapo kuwa
hajapokea ripoti ya escrow na kuwa akiipokea ataikabidhi kwa Bunge kama
inavyotakiwa.
Pinda alitoa maelezo kuhusu ripoti ya CAG, ambayo
ilikuwa kwenye swali la msingi la Mbarouk aliyetaka tamko la Serikali
kujua kwa nini wahisani wamegoma kutoa fedha za maendeleo nchini.
Pinda alisema wafadhili mara nyingi wanakuwa na
sababu mbalimbali, hilo unalozungumza itakuwa ni kesi iliyotokea safari
hii, lakini miaka miwili iliyopita kumekuwa na manung’uniko ya kuchelewa
kwa fedha hizo, lakini hili la sasa wanasema wanasubiri waone ripoti ya
CAG itolewe na ibainike yaliyomo katika ripoti hiyo na wao kama
wataridhika watatoa hizo fedha.
“Mimi nasema inshaallah, yatabainika na ni
matumaini yangu watatoa hizo fedha, jambo linalonisononesha ni pale
unapokuwa katika uamuzi wake unaoweza kugusa watu watatu, wanne, lakini
unafanya uamuzi ambao unakwenda kuathiri jamii ya Watanzania wengi hasa
wale wa vijijini.
No comments
Post a Comment